Brian Chesky
Habari zenu, naitwa Brian. Kwa mwaka uliopita, nimekuwa nikikaribisha wageni nyumbani kwangu hapa San Francisco na nimekutana na watu wazuri sana na tumefurahia ushirika pamoja. Mojawapo ya mambo nipendayo ni kuota moto mekoni. Nadhani Sophie hufurahia hilo zaidi yangu.
[Muziki wa mdundo]
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian anazungumza moja kwa moja kwenye kamera uso wake ukionekana kwa ukaribu, akitabasamu. Anapozungumza, tunaona picha za matukio aliyoshiriki na wageni wake: kwanza, ameketi mezani sebuleni mwake, akifurahia chakula cha jioni cha saladi na watu 2. Kisha, yuko kwenye baraza lake, ameketi kwenye kiti cha mikono, akizungumza na wanandoa wanaotazama upande wa pili. Sophie, mbwa wake aina ya Golden Retriever, anapapaswa kwa wororo. Mandhari yanabadilika kukiwa na watu walewale, huku Sophie akikaziwa uangalifu na nyuma ya Brian na wageni wake, meko yanaangaza mwanga. Mezani, kuna sahani ya biskuti. Mwishowe, mahali palepale lakini akiwa na mgeni tofauti, picha iliyo na mwangaza hafifu inaangazisha meko. Brian anakula biskuti huku Sophie akiangalia sahani kwa makini, mgeni akimwangalia kwa uangalifu.
Brian Chesky
Ila jambo moja lisilofurahisha ni kusimamia tangazo langu. Programu ni ngumu sana kutumia. Kama unavyojua, kusimamia tangazo ni moja ya mambo muhimu katika kukaribisha wageni. Hivyo ndivyo wageni hupata habari kuhusu nyumba yako. Tumeona kwamba matangazo yenye maelezo zaidi yanaweza kuwekewa nafasi hadi asilimia 20 zaidi. Lakini kuweka maelezo kwenye tangazo lako ni vigumu sana.
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian anaongea kwenye kamera, picha mbili zinabadilishana nafasi. Katika picha pana, tunaona kifupi mazingira yake: anaketi mbele ya meza ya mviringo ya mbao, simu yake ikiwa juu yake. Kushoto mwa skrini kuna ukuta wenye rangi nyepesi ulio na mchoro kwenye fremu ya mbao, pamoja na kabati fupi la mbao linaloonyesha ua jeupe na taa ya mviringo yenye mwanga hafifu. Upande wa kulia wa skrini, kuna ukuta ulio na ramani ya dunia, kiti kifupi kilicho na mto wenye umbo la neno kama "Airbnb," taa ya sakafuni, dawati la mbao la mtindo wa Skandinavia pamoja na kiti na mapambo fulani.
Picha ya pili inavutwa karibu kwenye uso wa Brian Chesky, ikizingatia nywele zake zilizopambwa vizuri na fulana nyeusi.
Brian Chesky
Hebu nikupe mfano. Tuseme nataka kuweka meko yangu. Kwanza, nitahitaji kutafuta tangazo langu. Liko hapa mahali fulani. Sawa kabisa. Kisha, inabidi niende kwenye Vistawishi. Na sasa ninaanza kuvinjari na kuvinjari. Na bado sijalipata. Hii inapaswa kuwa rahisi sana. Basi tunajiuliza, vipi tukifanya usimamizi wa tangazo lako kuwa rahisi sana na ifurahishe kufanya hivyo?
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian anachukua simu mkononi mwake na skrini inavuta karibu. Skrini inaonyesha ujumbe kama "Karibu tena, Brian!", "Nafasi ulizoweka" na maelezo mbalimbali ya nafasi zilizowekwa. Anabofya kitufe chenye mistari mitatu mlalo kwenye kona ya chini kulia kisha anachagua tangazo lake. Sehemu iliyoangaziwa inaonekana, iliyoandikwa "Kuhusu tangazo," ikionyesha picha na maelezo ya ziada.
Wakati huu, anaelekea kwenye sehemu ya "Vistawishi" na anaanza kusogea, akionyesha changamoto ya kupata kile anachotafuta. Mwishowe, anaweka simu mezani na kamera inavuta karibu uso wake.
Brian Chesky
Hivyo ndivyo tumefanya. Tunakuletea kichupo cha Matangazo. Njia rahisi ya kusimamia tangazo lako na kuonyesha nyumba yako. Sasa, unapogusa kichupo cha matangazo, kitu cha kwanza unachoona ni tangazo lako. Ili kuhariri tangazo langu, ninachohitaji kufanya ni kulibofya tu. Nipo ndani ya kihariri cha tangazo langu, ambacho kimegawanywa katika sehemu mbili: "Sehemu yako" na "Mwongozo wa kuwasili."
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian anapoongea kwenye kamera, mandharinyuma inafifia na kuwa nyeupe na mistari miekundu inayokingamana inaonekana na kuunda ikoni ya nyumba. Chini ya alama hii, imeandikwa "Matangazo." Kama inavyoonekana, alama hii hutumika kama kitufe katikati ya upau wa chini ndani ya programu ya Airbnb.
Kufungua ikoni hii huonyesha maudhui ya "Matangazo," yaliyopangwa vizuri katika vichupo viwili: "Sehemu yako" na "Mwongozo wa kuwasili." Chini ya vichupo hivi, kiashiria cha hali cha kijani kinasema kwamba nyumba hiyo imetangazwa.
Brian Chesky
Hebu tuanze na sehemu yako. Hapa ndipo unaweka maelezo yote kuhusu nyumba yako, kama vile kichwa chako, maelezo na vistawishi. Unakumbuka jinsi ilivyokuwa vigumu kuweka meko yangu? Naam, sasa ninabofya tu alama ya kujumlisha. Ninachagua aina ninayotaka. Meko yangu iko nje, ndiyo ile pale.
Maelezo Kuhusu Maonyesho
Sehemu iliyotengwa inaruhusu upakiaji wa picha ili kuunda ziara ya picha. Chini zaidi kwenye skrini, tunakuta jina la tangazo. Skrini inavyoendelea kuteleza, maelezo zaidi yanaonekana, kama vile aina ya nyumba, nafasi za wageni, maelezo ya kina, vistawishi na orodha ya vipengele vya ufikiaji. Brian anazungumza akiangalia kamera, akiuliza swali.
Baada ya hapo, ndani ya programu, chini ya kichupo kilichoandikwa "Sehemu yako," unabofya "Vistawishi," ukigusa alama ya kujumlisha hapo juu kulia mwa skrini. Inafunua msururu wa vitufe vya kuchuja aina. Baadhi yake ni pamoja na Vitu vya msingi, Bafu, Burudani, Huduma na Nje. Brian anachagua hiki cha mwisho na machaguo kadhaa yanatokea, ikiwemo Ua wa nyuma, Meko na Fanicha za nje.
Brian Chesky
Hebu tuongee kuhusu picha, ambazo ni mojawapo ya sehemu muhimu zaidi za tangazo zuri.
Hivi ndivyo wageni huziona kwa kawaida. Ni orodha moja ndefu. Lakini ziara ya picha ni bora zaidi. Hupanga picha zako katika vyumba ili kuwapa wageni uelewa mzuri wa nyumba yako.
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian Chesky anaendelea na sauti yake ya kushawishi anapoongea akitazama kwenye kamera. Ndani ya programu, tunashuhudia usogezaji laini kupitia mkusanyo wa picha unaoonyesha vyumba mbalimbali katika nyumba iliyotangazwa ya Brian.
Ingawa picha hizi zinajaza sehemu zote, mpangilio wake unaweza kuonekana kama mparaganyo. Hata hivyo, ndani ya kipengele cha hivi karibuni cha programu, tunaona ziara ya picha iliyopangwa kwa uangalifu chumba kwa chumba. Juu ya skrini, tutaona vijipicha kwa uteuzi rahisi wa chumba na chini yake kidogo, picha za sehemu iliyochaguliwa zinaonyeshwa kwa namna inayoonekana zaidi na iliyopangwa vizuri. Tunapoendelea kusogeza chini, tutakuta maonyesho safi na yanayoeleweka ya picha zote za kila chumba.
Brian Chesky
Shida ni kwamba kuunda ziara ya picha ni ngumu sana. Na kwa sababu hiyo, ni asilimia 10 tu ya matangazo yaliyo nayo. Hadi hivi karibuni, hata mimi sikuwa nayo. Lakini sasa unachohitaji kufanya ni kubofya tu na kutengeneza ziara yako ya picha. Tumejenga injini mahususi ya AI inayochambua picha zako zote na kuzipanga kimahiri ndani ya vyumba. Kisha, ziara yangu ya picha imekamilika. Lo! Kwa kweli ni kama miujiza.
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian Chesky anapoendelea kuzungumza, kamera inabadilika kati ya picha mbili zilizotajwa hapo awali. Anashikilia simu yake kwenye mkono wake wa kulia, akionyesha mawazo yake kwa shauku kupitia ishara za uso.
Tunapoelekea kwenye skrini ya programu, tunakuta Kihariri cha Tangazo, chenye kisanduku kwenye nusu ya chini kinachosema "Onyesha picha zako kulingana na chumba, papo hapo." Vijipicha vitatu hutumika kama mifano na chini yake, kitufe cheupe kinadokeza uundaji wa ziara ya picha. Kubofya kitufe hiki kunafunua picha inayoonyesha picha kadhaa zilizopangwa, pamoja na maandishi "Kupanga picha zako katika vyumba." Picha zinahuika, zinabadilika ukubwa, zinapishana na kupangwa katika miraba minne yenye ukubwa sawa. Baada ya uhuishaji kumalizika, tunasoma: "Ziara yako ya picha iko tayari!" Chini ya hapo, kwa herufi nyeupe kwenye kitufe cheusi: "Angalia!" Kubofya kitufe hiki husababisha uhuishaji mfupi wa kusherehekea na ziara ya Picha iliyokamilika. Mvuto mfupi wa karibu huonyesha picha zikiwa karibu.
Brian Chesky
Kwa mara ya kwanza, unaweza pia kuweka vistawishi kwenye kila chumba. Ukipenda kuweka chumba kingine, fanya hivyo wakati wowote. Nami napenda hii: tumeunda ikoni hizi mahususi zenye kuvutia kwa vyumba na sehemu 40 tofauti. Ni nzuri sana. Angalia ulaini wa kitambaa. Kiwango cha undani ni cha kushangaza na kiwango hiki cha undani ni dhihirisho la umakinifu tuliotumia katika kubuni mambo haya yote.
Maelezo kuhusu maonyesho
Katika programu, tunapoangalia picha kwa karibu, mraba ulioandikwa "Chumba cha kulala" unabofya na kusogeza chini taratibu ili kuchagua "Vistawishi." Kichwa kinaonekana: "Kuna nini kwenye chumba hiki?" na machaguo kama vile Mashuka ya kitanda, Mito na blanketi za ziada na mapazia ya kutia kiza kwenye Chumba. Mbili za mwisho zimechaguliwa.
Kisha, tukirudi kwenye picha ya Brian akizungumza kwa shauku, huku ikoni mahususi zikitajwa, skrini inaonyesha mkusanyo wa ikoni mahiri za 3D. Moja inapanuka na kujaza skrini, ikionyesha sofa yenye mdoli na mito miwili juu yake. Mvuto wa karibu wa picha unaonyesha mambo ya kina ya kushangaza katika misokotano hiyo.
Brian Chesky
Hivyo ndivyo unavyohariri sehemu yako. Sasa, baada ya mgeni kuweka nafasi, ni muhimu ajue nini cha kufanya anapowasili. Ila kuweka maelezo haya kumekuwa vigumu sana kwani yametawanyika kote kwenye programu. Ila sasa mambo ni tofauti. Bofya Mwongozo wa kuwasili. Unaweza kuweka maelezo haya katika sehemu moja, ikiwemo maelezo ya Wi-Fi, mwongozo wako wa nyumba na maelekezo ya kuingia.
Maelezo kuhusu maonyesho
Huku Brian Chesky akiendelea kuzungumza, kamera zinaonyesha picha pana ya uso wake na kuturuhusu kuona mazingira. Inabadilishana na picha fupi zilizopigwa kutoka pembe tofauti.
Kisha, tunahamia kwenye skrini ya programu ndani ya Kihariri cha Tangazo. Kichupo cha "Sehemu yako" kinachaguliwa na hali ya "Imetangazwa" inaonyeshwa kwa nukta ya kijani kibichi.
Kwa kubadilisha vichupo kwenda "Mwongozo wa kuwasili," tunakuta kichwa "Njia ya kuingia" pamoja na maneno "Weka maelezo" yaliyoandikwa kwa herufi za kijivu chini yake. Katika kuondoka kwenye picha ya skrini nzima, tunaona chaguo la "Unganisha kufuli lako kwa ajili ya kuingia kwa urahisi," maelezo kuhusu Wi-Fi, Mwongozo wa nyumba na Sheria za nyumba.
Brian Chesky
Basi, hebu tuzungumze kuhusu kuingia. Kama nyinyi, mimi pia nina kufuli janja. Sasa tunarahisisha mchakato wa kutumia njia moja kupitia ujumuishaji wa Kufuli Janja. Ninachohitaji tu ni kuingia kwenye akaunti yangu ya Kufuli Janja moja kwa moja kutoka kwenye programu ya Airbnb nami ninaunganishwa. Programu ya Airbnb itaunda kiotomatiki msimbo wa kipekee kwa kila nafasi iliyowekwa. Misimbo hii inatumika tu wakati wa safari ya mgeni na unaweza kuweka muda wa ziada kutokana na kile kinachokufaa wewe na mgeni wako. Utaweza kuanza kutumia Kufuli Janja nchini Marekani na Kanada baadaye mwaka huu.
Maelezo kuhusu maonyesho
Kuhusu ujumuishaji wa Kufuli Janja, tunaangalia nusu ya juu ya kichupo cha "Mwongozo wa kuwasili". Kubofya "Unganisha kufuli lako kwa ajili ya kuingia kwa urahisi" kunaongoza kwenye skrini nyingine inayoonyesha kicharazio cha nambari na ikoni ya kufuli lililofungwa kwenye sehemu ya juu, kukiwa na kichwa chini. Ndani ya sehemu ya ndani ya skrini, kuna kitufe cheusi chenye herufi nyeupe zinazosema "Unganisha" na chini yake, chaguo la "Endelea bila kuunganishwa."
Baada ya kubofya kitufe, tunaonyeshwa chaguo la kuchagua kufuli letu, kukiwa na machaguo matatu ya chapa: Schlage, Yale na August. Ndani ya kila chapa, majina ya miundo tofauti ya kufuli yameorodheshwa. Baada ya kuchagua moja, ishara ya sauti inalingana na uhuishaji wa kufuli janja, ikionyesha muunganisho uliofanikiwa. Mkusanyo wa picha za kufundishia unaanza kuhuishwa.
Picha ya kwanza ina kichwa: "Tutashughulikia kushiriki misimbo na wageni." Ndani yake, mfuatano nasibu wa nambari 4 unaundwa huku Brian Chesky akitaja kwamba kila nafasi iliyowekwa itakuwa na msimbo wa kipekee.
Kisha, kuna kalenda inayoonyesha "Kuingia" na "Kutoka" yenye kichwa "Misimbo inatumika tu wakati wa safari ya mgeni."
Baada ya hapo kuna kalenda yenye sehemu ya kwanza ikiwa nyeusi, katikati ni kijivu na ya mwisho ni nyeupe. Neno "Kutoka" linaonyeshwa kati ya sehemu mbili za kwanza na kati ya sehemu za kijivu na nyeupe, "Msimbo utakwisha muda wa kutumika." Kichwa kinasema: "Misimbo inakwisha muda wa kutumika dakika 30 baada ya kutoka."
Sehemu hiyo inahitimishwa na Brian akizungumza akiangalia kamera tena.
Brian Chesky
Na sasa, kwa mara ya kwanza, unaweza kuona mwongozo wako wa kuwasili kama mgeni wako atakavyouona. Unachohitaji kufanya bofya "Angalia". Ndiyo hiyo. Hicho ni kichupo kipya cha matangazo kukiwa na kihariri tangazo kipya kinachoonyesha sehemu yako na mwongozo wa kuwasili, ziara ya picha inayowezeshwa na AI na ujumuishaji wa Kufuli Janja.
Maelezo kuhusu maonyesho
Brian Chesky anazungumza kwa unyoofu, macho yake yakiangazia kamera.
Tunahamia kwenye skrini ya programu, ndani ya sehemu ya "Mwongozo wa kuwasili", ambapo tunaona nyakati za kuingia na kutoka pamoja na taarifa nyingine. Kuna ikoni ya betri ya kijani karibu na chaguo la Kufuli Janja. Kwenye sehemu ya chini, kuna kitufe cheusi chenye ikoni ya jicho inayosema "Tazama" kwa rangi nyeupe. Kwa kuibofya, tunaona nyumba iliyotangazwa iliyo na picha (katika hali hii, kitanda kilicho na blanketi lenye rangi nyingi katika chumba kilicho na madirisha mawili ya wima mbele ya kitanda, fremu ya picha na mimea fulani). Baada ya kumaliza maelezo, kamera inarudi kwa Brian huku akiweka simu mezani taratibu.
Kwenye skrini ya programu, tunaona kwa ufupi vichupo "Sehemu yako" na "Mwongozo wa kuwasili." Simu imewekwa upande wa kushoto wa skrini dhidi ya mandharinyuma nyeupe. Kwenye simu nyingine, upande wa kulia wa ile ya kwanza, tunaona chaguo la "Ziara ya Picha" pamoja na uhuishaji wake wa kusherehekea. Kwenye simu ya tatu upande wa kulia wa picha, tunaona skrini inayoonyesha ujumuishaji wa Kufuli Janja.
Brian Chesky
Tulianza mradi huu zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Tulileta baadhi ya wabunifu na wahandisi bora zaidi ulimwenguni na kile walichounda labda ni jambo bora zaidi ambalo tumewahi kubuni. Kuna sababu rahisi ya kuweka nguvu kubwa katika hili: kwa sababu tunajua ili uwe mwenyeji mzuri, unahitaji nyenzo bora. Ni matumaini yangu kwamba utaipenda. Natamani sana uijaribu.
Maelezo kuhusu maonyesho
Katika picha tofauti za Brian Chesky akizungumza akiangalia kamera kutoka umbali na pembe mbalimbali, tunaona kwamba anatumia ishara kusisitiza maneno yake anapoelezea. Anahitimisha kwa tabasamu la uhakika, lenye kung'aa.